Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo katika mkutano wake na wazalishaji na wadau wa viwanda vya petrokemikali na chuma hapa nchini. Amesema kuwa, maadui wa Jamhuri ya Kiislamu wanadhani kuwa, baada ya vikwazo na vita vyao vya kiuchumi dhidi ya taifa la Iran, Tehran italazimika kuwasiliana na kufanya mazungumzo nao na kuongoza kuwa: Katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili iliyopita ya utekelezaji wa vikwazo vikali zaidi vya kiuchumi vya maadui, Wamarekani wenyewe wameomba kufanya mazungumzo na Iran tena mara kadhaa.
Rais Rouhani amesema kuwa, kujitosheleza katika uzalishaji wa sekta ya petrokemikali na chuma ni mafanikio muhimu kwa Iran. Ameongeza kuwa, hii leo serikali inajifakharisha kwamba, imeweza kusimama kidete mbele ya vikwazo na mashinikizo ya kigeni na kwamba kusimama imara huko kumewezekana kwa msaada na jitihada kubwa za wazalishaji wote, wawekezaji na wachapakazi hususan katika sekta ya petrokemikali na chuma.
Amesema kuwa uzalishaji wa petrokemikali na chuma umechangia sana katika pato la nchi kutokana na bidhaa zisizo za mafuta na kwamba bidhaa hizo kutoka Iran zinachuana na bidhaa za wazalishaji wengine katika masoko ya kimataifa.
342/